Shehena ya kwanza ya chanjo ya Mpox imewasili jana nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Akizungumza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa N’djili, mjini Kinshasa, Waziri wa Afya nchini humo Roger Kamba amesema, wamepokea dozi 99,100 jana, na nyingine zinatarajiwa kuwasili nchini humo kesho, na kuongeza kuwa, nchi hiyo inajitahidi kudhibiti ugonjwa huo haraka iwezekanavyo, hususan katika mikoa iliyoathiriwa zaidi ya Kivu Kusini na Equateur.
Pia Bw. Kamba amesema, Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) litashughulikia kampeni ya utoaji wa chanjo katika mikoa iliyoathirika zaidi, lakini hakuweka wazi tarehe rasmi ya kuanza kutolewa kwa chanjo hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na UNICEF hivi karibuni, DRC ambayo ilitangaza mlipuko wa Mpox mwishoni mwa mwaka 2022, imeripoti zaidi ya kesi 18,000 zinazoshukiwa kuwa ugonjwa huo, ikiwemo vifo 629 tangu mwanzo wa mwaka huu, huku watoto wanne wakiwa miongoni mwa watu waliofariki kutokana na ugonjwa huo.