Rais Xi Jinping wa China amemtumia salamu za pongezi kiongozi mkuu wa Korea Kaskazini Bw. Kim Jong Un kutokana na Maadhimisho ya Miaka 76 tangu kuanzishwa kwa nchi yake.
Katika salamu hizo, rais Xi ameeleza kuwa, anaamini chini ya uongozi wa chama tawala cha Wafanyakazi kinachoongozwa na Bw. Kim Jong Un, watu wa Korea Kaskazini watapata mafanikio makubwa zaidi katika mchakato wa kuhimiza mambo ya ujamaa wenye umaalumu wa Korea Kaskazini.
Rais Xi pia amesisitiza kuwa, kutokana na hali mpya katika zama mpya, China itaendelea kuuchukulia uhusiano kati yake na Korea Kaskazini kwenye mtazamo wa kimkakati na muda mrefu, na inapenda kukuza mawasiliano ya kimkakati, kuimarisha uratibu na ushirikiano na Korea Kaskazini, kulinda, kuimarisha na kukuza uhusiano wa ushirikiano na urafiki wa jadi kati ya pande hizo mbili, kuhimiza kwa pamoja mambo ya ujamaa, ili kuwanufaisha zaidi watu wa nchi hizo mbili, na kutoa mchango mkubwa zaidi katika kuhimiza amani na utulivu, na maendeleo na ustawi wa kikanda na wa dunia.