Mji mkuu wa Ufaransa, Paris, utamuenzi mwanaolimpiki wa Uganda Rebecca Cheptegei, ambaye alichomwa moto na mpenzi wake, kwa kukipa jina kituo cha michezo kwa heshima yake, Meya wa Paris Anne Hidalgo alitangaza Ijumaa.
Mwanariadha huyo wa mbio za marathon, ambaye alishiriki katika Michezo ya Paris mwezi uliopita alifariki Alhamisi, siku nne baada ya kumwagiwa petroli na kuchomwa na mpenzi wake nchini Kenya, katika shambulio la hivi karibuni dhidi ya wanariadha wa kike nchini humo.
Msichana huyo mwenye umri wa miaka 33, ambaye alimaliza katika nafasi ya 44 katika michezo yake ya kwanza ya Olimpiki, aliungua moto kwa zaidi ya asilimia 75 ya mwili wake katika shambulio la Jumapili, vyombo vya habari vya Kenya na Uganda viliripoti.
"Alitushangaza hapa Paris. Tulimwona. Uzuri wake, nguvu zake, uhuru wake, na ilikuwa inawezekana uzuri wake, nguvu na uhuru ambao hakuweza kuvumilia mtu aliyefanya mauaji haya," Hidalgo aliwaambia waandishi wa habari.
"Paris haitamsahau. Tutautoa ukumbi wa michezo kwa ajili yake ili kumbukumbu yake na hadithi yake ibaki miongoni mwetu na kusaidia kubeba ujumbe wa usawa, ambao ni ujumbe unaobebwa na Michezo ya Olimpiki na Walemavu."
Cheptegei ni mwanamichezo mashuhuri wa tatu kuuawa nchini Kenya tangu Oktoba 2021.
Waziri wa Michezo wa Kenya Kipchumba Murkomen alielezea kifo cha Cheptegei kama hasara "kwa kanda nzima".