Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephone Dujarric amesema, Sudan na Chad zimekumbwa na mafuriko, huku Lesotho ikiathiriwa na ukame.
Kwa mujibu wa msemaji huyo, Ofisi ya kuratibu misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imeonya kuwa mvua kubwa na mafuriko vimewaathiri watu karibu laki tano katika majimbo ya Darfur Kusini, Bahari ya Shamu, Mto Nile na Kaskazini nchini Sudan tangu mwezi Juni, na kufanya hali ya kibinadamu nchini humo iwe mbaya zaidi.
Nchini Chad, OCHA imesema mafuriko yamesabibisha vifo vya watu wasiopungua 340 na kuwaathiri watu karibu milioni 1.5, huku nyumba zaidi ya laki 1.6 zikiwa zimeharibiwa.
OCHA pia imeripoti kuwa hali ya usalama wa chakula nchini Lesotho inazidi kuwa mbaya kufuatia ukame wa kihistoria uliosababisha na athari za El Nino.