Maofisa wa ulinzi wa Kenya wametoa mwito wa kulinda maeneo ya mipakani ya Afrika dhidi ya matishio mbalimbali, ikiwa ni pamoja na majanga ya tabianchi, biashara ya binadamu, migogoro na uhalifu wa kuvuka mipaka, ambayo yanahitaji utafiti wa pamoja na kubadilishana mbinu bora.
Wakizungumza mjini Nairobi kwenye Mkutano wa mwaka wa Mtandao wa utafiti kuhusu maeneo ya mpakani ya Afrika, maofisa hao wamesema kuimarisha usalama katika mipaka ya bara hilo kunategemea kutumia maarifa na data za kitaalamu.
Makamu mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, John Omenda, amesema kupitia utafiti shirikishi, watunga sera wa Afrika wanaweza kupata ufahamu kuhusu uhusiano kati ya amani, usalama na maendeleo.
Watunga sera, maofisa wa ulinzi, wawakilishi wa wakopeshaji wa pande nyingi, na wasomi walihudhuria mkutano huo, uliotoa jukwaa la kubadilishana matokeo ya utafiti kuhusu kuboresha usalama wa mipaka ya Afrika.