Wafanyakazi wa usafiri wa ndege wa Kenya wasitisha mgomo baada ya kufikia makubaliano na mamlaka husika
2024-09-12 10:24:35| CRI

Wafanyakazi wa usafiri wa ndege wa Kenya wamemaliza mgomo wao wa siku moja baada ya kufikia makubaliano ya kurejea kazini na mamlaka husika.

Muungano wa wafanyakazi wa usafiri wa ndege (KAWU),Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ya Kenya (KAA), Shirika la Ndege la Kenya (KQ), na maofisa wa serikali wamesaini makubaliano yanayoruhusu shughuli za kawaida za safari za ndege kuanza tena kote nchini Kenya.

Mgomo huo ulitatiza shughuli katika viwanja vinne vya ndege nchini Kenya, na kusababisha usumbufu mkubwa wa usafiri. Katibu Mkuu wa KAWU Bw. Moses Ndiema amesema huduma katika viwanja vya ndege vya Kenya zitarejea katika hali ya kawaida.

Bw. Ndiema pia amesema wamepokea nyaraka muhimu kama walivyodai, na kwamba watazipitia ndani ya siku 10 za kazi, na kubainisha maeneo waliyo na wasiwasi nayo, ambayo yataelezwa mara moja kwenye mazungumzo na serikali.