Polisi ya Kenya imesema, wameimarisha ulinzi kote nchini wakati magaidi wakitoa vitisho vipya.
Akitoa taarifa Jumamosi usiku huko Nairobi, msemaji wa Huduma ya Polisi ya Taifa NPS Bw. Resila Onyango ameuhakikishia umma usalama wao kufuatia tahadhari ya kuaminika kwamba wapiganaji wa Al-Shabaab wanapanga mashambulizi mapya huko Nairobi, mji mkuu wa Kenya na miji mingine katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Bw. Onyango amesema maofisa wa Polisi wamesambazwa kote nchini wakiwa macho kulinda nchi hiyo ambayo imekuwa ikikabiliwa na matishio ya kigaidi yanayoongezeka kutoka kundi la Al-Shabaab.
Pia ameutaka umma kushirikiana na polisi kupitia kuripoti watu au vitendo vyovyote vyenye mashaka kwenye kituo cha polisi kilichoko karibu au kupiga namba za bure za kuripoti.