Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Patrice Motsepe alishukuru maandalizi ya awali ya Kenya kama mwandaaji mwenza wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Motsepe alitembelea viwanja vitatu jijini Nairobi, ambavyo vinafanyiwa ukarabati au vinajengwa kwa ajili ya maandalizi ya AFCON 2027 na mashindano ya Mataifa Bingwa ya Afrika (CHAN) 2025. Siku ya Jumapili, alikutana na Rais wa Kenya William Ruto kujadili hatua iliyofikiwa.
Wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumatatu baada ya kikao cha Kamati Tendaji ya CAF mjini Nairobi, Motsepe alionyesha imani katika uwezo wa Kenya wa kutoa miundombinu muhimu.
Kwa upande wake rais Ruto aliihakikishia CAF kuwa Kenya itakuwa tayari kuandaa michuano mizuri ya soka barani humo, licha ya kukosa uwanja ulioidhinishwa na CAF kwa sasa. Viwanja vya Kimataifa vya Michezo vya Moi na Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi ambavyo vimefungwa kwa ajili ya ukarabati ni miongoni mwa viwanja vinavyotengenezwa.
Kenya itaandaa kwa pamoja michuano ya CHAN na AFCON na majirani zake Uganda na Tanzania. Motsepe alitangaza kuwa CHAN 2025 itafanyika kuanzia Februari 1 hadi 28, huku mechi zikifanyika Nairobi, Kampala nchini Uganda, na Dar es Salaam nchini Tanzania.