Sudan yaripoti zaidi ya wagonjwa 9,500 wa kipindupindu, vifo 315
2024-09-17 08:57:27| CRI

Wizara ya Afya ya Sudan ilisema Jumatatu kwamba nchi hiyo imerikodi wagonjwa 9,533 wa kipindupindu, pamoja na vifo 315. Katika taarifa yake wizara hiyo ilisema kwamba kiwango cha maambukizi kinachoongezeka kwenye mlipuko wa hivi karibuni kilifikia watu 9,533 hadi juzi Jumapili.

Waziri wa Afya wa Sudan Haitham Mohamed Ibrahim alitangaza rasmi mlipuko wa kipindupindu nchini humo Agosti 17. Wizara hiyo ilihusisha kuenea kwa kipindupindu na kuzorota kwa hali ya mazingira iliyosababishwa na vita na matumizi ya maji machafu.

Tangu kuzuka kwa mapigano kati ya Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka mwezi Aprili 2023, magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu, malaria, surua na homa ya dengue yameenea, na kusababisha mamia ya vifo. Mzozo huo umesababisha vifo vya watu 16,650 na mamilioni ya watu kuhama makazi yao.