Watoto milioni 3.4 wako katika hatari kubwa ya kupatwa na magonjwa ya kuambukiza nchini Sudan
2024-09-18 08:47:33| CRI

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limesema katika taarifa yake kuwa takriban watoto milioni 3.4 wenye umri wa chini ya miaka mitano wako katika hatari kubwa ya kupatwa na magonjwa hatari ya kuambukiza nchini Sudan.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan Sheldon Yett alinukuliwa katika taarifa hiyo akisema kutokana na mvua kubwa na mafuriko nchini humo, magonjwa kama vile kipindupindu, malaria, homa ya Dengue, surua na rubela yanaweza kuenea kwa kasi zaidi na kuharibu vibaya mustakabali wa watoto katika majimbo yaliyoathirika na kwingineko.

Amesema msukosuko huo unatokana na kushuka kwa kiwango kikubwa cha chanjo na uharibifu wa miundombinu ya afya, maji, vyoo na usafi kutokana na mzozo wa ndani unaoendelea, na kuongeza kuwa kuzorota kwa hali ya lishe ya watoto wengi nchini Sudan kunawaweka katika hatari kubwa zaidi.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa UNICEF iliwasilisha dozi 404,000 za chanjo ya kipindupindu nchini Sudan Septemba 9.