Kwa mujibu wa takwimu mpya za kiuchumi zilizotolewa Jumanne na Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Kenya (KNBS) mjini Nairobi, mapato ya Kenya kutokana na mauzo ya nje ya kilimo cha bustani yamepungua kwa asilimia 3.5 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, kutokana na kupungua kwa usafirishaji kwenda kwenye masoko ya Ulaya na Asia.
KNBS imesema, nchi hiyo ilipata shilingi bilioni 86.8 (takriban dola za Kimarekani milioni 673) katika kipindi hicho, zikipungua ikilinganishwa na dola milioni 697 katika kipindi kama hicho mwaka 2023. Katika miezi sita ya kwanza ya 2024, Kenya iliuza nje tani 214,676 za maua, matunda na mboga, zikiwa chini ikilinganishwa na tani 291,118 katika kipindi kama hicho mwaka 2023.
Kupungua kwa mapato katika nusu ya kwanza ya mwaka huu kumechangiwa kwa kiasi fulani na kuimarika kwa shilingi ya Kenya, ambayo ilifanya mauzo ya nje kuwa ghali zaidi na kupunguza mahitaji.