Kenya yajihatarisha kwa WADA baada ya kupunguza bajeti kwa wakala wa kupambana na dawa za kusisimua misuli
2024-09-18 08:48:46| CRI

Kenya iko katika hatari ya kutangazwa kutotii sheria na Shirika la Kupambana na Matumizi ya Dawa za Kusisimua Misuli Duniani (WADA) baada ya serikali ya nchi hiyo kupunguza kwa kiasi kikubwa bajeti ya Shirika la Kupambana na Dawa za Kusisimua Misuli nchini Kenya (ADAK) kwa mwaka wa fedha wa 2024/25.

Akiongea na wanahabari mjini Nairobi, mwenyekiti wa ADAK Daniel Makdwallo alionya kwamba shirika hilo haliwezi kuendesha shughuli zake, baada ya kutengewa shilingi milioni 20 (dola 155,000 za Kimarekani) kutoka dola milioni 2.23 ilizopokea katika mwaka wa fedha uliopita.

Amebainisha kuwa wako katika hatari ya kutoweza kuandaa au kutuma mwanamichezo yeyote kwenye mashindano ya kimataifa kwa sababu Shirika haliwezi kufanya shughuli zake za kupima mara kwa mara katika mashindano na nje ya mashindano.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Shirika limewafungia wanariadha 78 kwa kukiuka Sheria ya Kupambana na Matumizi ya Dawa za Kusisimua Misuli, juhudi ambazo zilipongezwa na WADA na Kitengo cha Kusimamia Maadili ya Wanariadha (AIU).