Wizara ya Afya ya Lebanon imesema idadi ya waliouawa katika milipuko ya vifaa vya mawasiliano visivyotumia waya imeongezeka hadi 14, na wengine 450 wamejeruhiwa.
Milipuko ilisikika jana alasiri katika kitongoji cha kusini mwa Beirut na mikoa kadhaa iliyopo kusini na mashariki mwa Lebanon.
Ripoti za usalama zilionyesha kuwa mlipuko huo ulitokea katika kitongoji cha kusini mwa Beirut kwenye mazishi ya wanachama wanne wa Hezbollah, na mingine kama hiyo iliyozua moto katika magari na majengo ya makazi, na kusababisha majeraha kadhaa.
Vyombo vya habari vya Lebanon vilisema vifaa vilivyohusika vilitambuliwa kama ‘radio call’ aina ya ICOM V82. Hadi sasa Hezbollah haijazungumzia tukio hilo.
Milipuko hiyo ilifuatia shambulio la siku moja iliyopita, ambapo jeshi la Israel linadaiwa kulenga betri za kifaa cha kupokea ujumbe ‘pager’ zinazotumiwa na wanachama wa Hezbollah, na kusababisha vifo vya watu 12, wakiwemo watoto wawili, na takriban majeruhi 2,800. Katika taarifa iliyotoa Jumanne, Hezbollah iliishutumu Israel kwa "kuwajibika kikamilifu kwa uvamizi wa uhalifu ambao pia ulilenga raia," na kutishia kulipiza kisasi. Israel bado haijatoa maoni yoyote kuhusu milipuko hiyo.