Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah alisema katika hotuba yake kwa njia ya televisheni siku ya Alhamisi kwamba milipuko ya vifaa vya mawasiliano iliyotokea Jumanne na Jumatano kote nchini Lebanon ni "kitendo cha vita na tangazo la vita la Israel."
Amesema Israel "ilikiuka mistari yote miekundu," huku akiita matukio hayo ni mauaji ya kimbari na kwamba yanaendelea kuchunguzwa, ikiwa ni pamoja na vifaa vilivyotumika. Akibainisha kuwa mashambulizi hayo hayatadhoofisha Hezbollah, Bw. Nasrallah alisema watakuwa na nguvu na uwezo zaidi wa kukabiliana na hatari yoyote, akiwahakikishia watu kuwa mapambano ya Lebanon hayatasita hadi wakomeshe mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza.
Jeshi la Israel lilitangaza Alhamisi kuwa "mipango ya kuendeleza vita" nchini Lebanon dhidi ya Hezbollah imeidhinishwa, huku likianzisha wimbi jipya la mashambulizi ya mabomu kusini mwa Lebanon.
Waziri wa Afya wa Lebanon Firas Abiad alisema Alhamisi kuwa idadi ya watu waliouawa katika milipuko hiyo imeongezeka hadi 37, ambapo waliojeruhiwa ni 2,931. Hakuna maafisa wa Israel waliotangaza kuhusika na milipuko hiyo, ambayo Hezbollah ilidai kuwa ilitokana na Israel.