UM na AU waitaka Sudan Kusini kutekeleza majukumu yaliyosalia ili kuhakikisha amani ya kudumu
2024-09-20 08:50:07| CRI

Tume za Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, pamoja na Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo ya Afrika Mashariki IGAD zimetoa wito kwa viongozi wa Sudan Kusini kufanya kazi pamoja na kukamilisha masuala yaliyosalia ya uchaguzi na usalama ili kufikia amani ya kudumu.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa huko Juba nchini Sudan Kusini, mamlaka hizo zilitoa wito wa kuwepo kwa kasi mpya ya kutimiza ahadi kwa watu wa Sudan Kusini kufuatia kuongezwa kipindi cha mpito cha amani, zikiongeza kuwa ni muhimu kwa Vyama na Serikali ya Mpito ya Umoja wa Kitaifa kujitoa na kuweka mifumo, kutoa uhakika na rasilimali zinazohitajika ambazo zinaweza kuhakikisha utekelezwaji wa majukumu yaliyosalia kwa wakati na kwa ukamilifu.

Serikali ya mpito ya nchi hiyo Septemba 13 ilitangaza kuahirishwa kwa uchaguzi wa kitaifa na kuongeza kipindi cha mpito kwa miaka miwili baada ya kushindwa kutimiza masharti muhimu ya makubaliano ya amani. Hii ni mara ya pili kwa nchi hiyo iliyopata uhuru mwaka 2011, kuahirisha uchaguzi na kuongeza kipindi cha mpito kilichoanza Februari 2020.