Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua alisema Alhamisi kuwa serikali ya Kenya itaimarisha usalama katika Kaunti ya Lamu, eneo maarufu la utalii, ili kukabiliana na ugaidi na vitisho vingine, ikilenga kuvutia wageni wengi zaidi.
Ameeleza kuwa serikali imehamasisha vyombo vyote ya usalama katika kaunti ili kuhakikisha amani inakuwepo miongoni mwa wakazi. Kaunti ya Lamu kwa muda mrefu imekuwa uwanja wa vita vya magaidi, hivyo vyombo vya usalama vinawafuatilia kwa karibu, na watakabiliwa na madhara makubwa.
Alisema kuwa uwekezaji wa serikali katika usalama umesaidia kuzuia mashambulizi ya kigaidi Mombasa na miji mingine ya pwani inayojulikana kwa utalii wa fukwe. Vikosi vya usalama vya Kenya vimefanikiwa kudhibiti vitendo vya kigaidi katika maeneo ya karibu na mpaka wa Somalia na Msitu wa Boni, ulioko kusini mashariki mwa nchi hiyo karibu na visiwa vya Lamu katika Bahari ya Hindi.
Licha ya hatua za usalama kuongezeka, ripoti za kuwepo kwa wanamgambo na mashambulizi Lamu na mpakani zinaendelea. Eneo hilo limeshuhudia mashambulizi makali ya wanamgambo katika miaka ya hivi karibuni, ambayo yamesababisha vifo vya maafisa wa usalama na raia.