Kenya imeungana na jamii ya kimataifa kuadhimisha Siku ya Faru Duniani, huku ikiahidi kuimarisha hatua za kuokoa idadi ya Faru weusi nchini humo.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku hiyo yaliyofanyika kitaifa katika Kaunti ya Samburu, kaskazini mwa Kenya, Katibu wa kudumu wa Wizara ya Utalii na Wanyamapori nchini Kenya, Rebecca Miano amesema serikali imetekeleza matumizi ya teknolojia mbalimbali ikiwemo droni na ushahidi wa kimahakama ili kuongeza ulinzi wa Faru. Pia amesema, serikali imetenga rasilimali muhimu ili kusaidia ajira kwa maofisa zaidi wa sheria, hatua ambayo itatoa mchango mkubwa katika juhudi za kuokoa idadi ya Faru iliyopo sasa na wanyamapori wengine kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Amesema Kenya ni makazi muhimu ya Faru, ikiwa na asilimia 80 ya Faru weuzi wa mashariki wanaopatikana katika maeneo manane nchini humo.