Vijana wa nchi za Afrika Mashariki wamekutana nchini Uganda kwenye kongamano la Usimamizi wa Mtandao wa Internet la Afrika Mashariki (EAIGF), na kupata mafunzo kuhusu manufaa na fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye mtandao wa internet katika enzi hii ya kidijitali.
Kongamano hilo la 11 limefanyika kwa siku mbili mjini Kampala, chini ya kaulimbiu ya Kujenga Mustakabali wa Kidijitali wa Wadau Mbalimbali kwa Vijana wa Afrika Mashariki. Kongamano limelenga kujenga uelewa wa pamoja wa masuala ya usimamizi wa mtandao wa Internet katika nchi za Afrika Mashariki na kuwezesha ushiriki wa maana katika sera ya kimataifa ya mtandao, usimamizi na maendeleo.
Mratibu wa miradi katika Jumuiya ya wanamtandao wa Uganda Bi. Beatrice Kayaga, amesema mitazamo ya vijana kuhusu usimamizi wa mtandao wa internet ni muhimu na lazima vijana washiriki kikamilifu katika michakato ya kufanya maamuzi ili kuhakikisha sauti zao zinasikika na mahitaji yao yanazingatiwa.