Wizara ya Afya ya Lebanon jana Jumatatu imetoa taarifa kuwa, watu 492 wakiwemo watoto 35 na wanawake 58 wameuawa, na wengine 1,645 kujeruhiwa katika mashambulizi makubwa ya anga ya Israel nchini humo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Lebanon, mashambulizi ya Israel katika kitongoji cha Beirut, mji mkuu wa Lebanon, yalimlenga ofisa mwandamizi wa kundi la Hezbollah la nchi hiyo. Hata hivyo Kundi la Hezbollah limetoa taarifa ikisema, mlengwa wa mashambulizi hayo ni Ali Karaki, ambaye hivi sasa amehamishwa katika sehemu salama.
Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel Rear Admiral Daniel Hagari amesema, jeshi la Israel lilishambulia maeneo zaidi ya 1,300 yaliyolengwa ya kundi la Hezbollah la Lebanon ndani ya saa 24 zilizopita.