Cote d'Ivoire yatarajia wawekezaji kuendeleza sekta ya korosho
2024-09-24 23:28:39| cri

Katika ufunguzi wa kongamano la uwekezaji kwa sekta ya korosho, lililofanyika Jumatatu mjini Abidjan, Waziri wa Kilimo, Maendeleo Vijijini na Uzalishaji wa Chakula wa Cote d'Ivoire Kobenan Kouassi Adjoumani amewahimiza wawekezaji wa kitaifa na kimataifa kuwekeza katika sekta ya korosho nchini humo.

Waziri huyo amesisitiza kuwa uzalishaji wa kila mwaka wa korosho nchini Cote d'Ivoire umeongezeka kwa kiasi kikubwa, na kuongezeka kutoka tani laki 5 za mwaka 2013 hadi tani milioni 1.2 mwaka 2023. Ukuaji huu ni matokeo ya programu na miradi kadhaa ya serikali inayolenga kuipa nguvu sekta ya korosho na kukuza uwekezaji.

Hata hivyo, amesema kuwa thamani iliyoongezwa kutoka kwa uchakataji wa bidhaa hii ndani ya nchi bado haijatumiwa kwa kiasi kikubwa. Mwaka 2023, ni asilimia 21 tu ya korosho ndiyo ilichakatwa ndani ya nchi, ambayo ni mbali na lengo la serikali la kufikia asilimia 50 ya uchakataji wa ndani ifikapo mwaka 2030.