Watu 41 wamefariki kutokana na ugonjwa wa surua nchini Sudan Kusini kuanzia mwezi Januari mwaka huu, huku kesi 3,160 zinazoshukiwa kuwa na ugonjwa huo zikiripotiwa.
Ripoti ya pamoja iliyotolewa jana na Wizara ya Afya ya Sudan Kusini pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) imesema, kesi zinazoshukiwa kuwa na surua ziliongezeka kwa kasi mwezi Machi, na hakuna kesi zilizothibitishwa kuwa na ugonjwa huo zilizoripotiwa kwa tangu mwezi Julai.
WHO imesema kampeni ya kutoa chanjo ya ugonjwa huo imefanyika katika kaunti 15, huku watoto 544,104 wakipatiwa chanjo dhidi ya ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi kubwa ya kesi zinazoshukiwa kuwa na surua ni kundi la watoto walio na umri wa chini ya mwaka mmoja, ambao asilimia kubwa hawakupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo.