Maonyesho ya Biashara ya Maisha ya Nyumbani ya China ya mwaka 2024 yameanza jana mjini Johannesburg, Afrika Kusini, na kampuni zaidi ya 400 zimeonyesha bidhaa na huduma zao kwa wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Ofisa mwendeshaji mkuu wa Maonyesho ya Kimataifa ya Meorient ambao pia ni waandaaji wa maonyesho hayo, Binu Pillai amesema, tamasha hilo lina mabanda zaidi ya 800 yakionyesha zaidi ya bidhaa 14,000 za ubora wa juu, huku watu 30,000 wakijiandikisha kushiriki. Amesema maonyesho hayo yanatoa fursa kwa kampuni za China na za Afrika kukutana na kufanya majadiliano ya kibiashara.
Pillai amesema, washiriki wa maonyesho hayo kutoka China wamepeleka bidhaa mbalimbali zenye ubora wa juu, ikiwemo mashine, vifaa vya biashara, vitambaa na nguo, vifaa vya matumizi ya nyumbani, na samani za ofisini.