Wapatanishi wa Afrika wakutana nchini Kenya kuandaa msimamo wa pamoja kabla ya mkutano wa mabadiliko ya tabianchi
2024-09-25 08:40:15| CRI

Zaidi ya wapatanishi 100 wa Afrika jana wameanza mkutano wa siku nne jijini Nairobi, Kenya, kuandaa mpango wa awali kabla ya Mkutano wa 29 wa Nchi Zilizosaini Makubaliano ya Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP29) utakaofanyika Baku, Azerbaijan, mwezi Novemba mwaka huu.

Kiongozi wa Timu ya Kundi la Wataalamu Wapatanishi wa Afrika (AGNES) George Wamukoya amesema, wapatanishi hao wanatathmini machaguo na kuandaa msimamo wa pamoja wa Afrika kabla ya mkutano wa COP29.

Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Wabunge wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, Emile Guirieoulou kutoka nchini Cote d’Ivoire amesema, wabunge wameunga mkono hatua halisi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi barani Afrika kupitia kutunga sera na kanuni sahihi.