Afisa wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kupanua mwitikio wa kibinadamu kwa Sudan
2024-09-26 14:03:55| cri

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Kibinadamu ambaye pia ni Naibu Mratibu wa Misaada ya Dharura Bi. Joyce Msuya, amesema Sudan inakabiliwa na msukosuko wa kibinadamu ambao haujawahi kushuhudiwa katika historia. Ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kupanua mwitikio wa kibinadamu kwa nchi hiyo.

Ameongeza kuwa mgogoro wa kisilaha nchini Sudan umedhoofisha huduma za msingi za umma nchini humo, zikiwemo huduma za afya, elimu, maji, na mitandao ya mawasiliano, na pia umesababisha moja ya misukosuko mikubwa zaidi ya watu kuhama makazi yao, nusu ya watu wa Sudan ikiwa ni takriban watu milioni 25.6, wanakosa usalama wa chakula, na karibu watoto milioni 5 chini ya umri wa miaka 5, wanawake wajawazito na kina mama wanaonyonyesha wanakabiliwa na utapiamlo mkali.

Bi. Msuya ametangaza kutengwa kwa dola za kimarekani milioni 25 kutoka Mfuko Mkuu wa Dharura wa Umoja wa Mataifa ili kukabiliana na uhaba wa chakula nchini Sudan. Ameitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza misaada ya kifedha kwa Sudan ili mwitikio wa kibinadamu uendelee kupanuka.