Umoja wa Afrika (AU) umesisitiza haja ya kufanyia mageuzi mifumo ya elimu barani Afrika kuelekea kutoka elimu bora na nyumbufu kwa wote.
Taarifa iliyotolewa na Umoja huo imesema, kauli hiyo imetolewa wakati wa mkutano uliofanyika jumatano chini ya kaulimbiu “Kuwekeza katika Kesho: Mwaka wa Umoja wa Afrika wa Mkakati wa Kuchochea Elimu kwa Afrika na Dunia.”
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amesisitiza haja muhimu ya kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora kwa Waafrika wote, huku lengo kuu likiwa ni katika makundi yaliyo hatarini zaidi, hususan wasichana na watu wenye ulemavu.
Kuhusu sekta ya elimu barani Afrika kuathiriwa na ukosefu wa usalama unaotokana na mapigano, Bw. Mahamat ametoa wito wa ulinzi wa taasisi za elimu na kusisitiza kuwa elimu inapaswa kutumika kama mwanga wa matumaini na injini ya maendeleo.
Aliyekuwa rais wa Tanzania Jakaya Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa Bodi ya Uhusiano wa Elimu Duniani, amesisitiza kuwa kuwekeza katika elimu ni uwekezaji unaohakikisha hatma nzuri kwa Afrika.