Makamu wa rais wa Uganda Jessica Alupo amesema China ni mwenzi wa kimkakati katika kuisaidia Uganda kuongeza kasi yake ya maendeleo.
Bi. Alupo amesema hayo katika hafla iliyoandaliwa jumatano wiki hii na Ubalozi wa China nchini Uganda mjini Kampala kuadhimisha miaka 75 ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China.
Makamu wa rais hiyo amesema licha ya ufadhili wa China uliotangazwa katika mkutano wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika hivi karibuni mjini Beijing, Uganda pia imesaini makubaliano ya ushirikiano na China ili kuimarisha biashara ya pande mbili.
Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa China nchini Uganda Zhang Lizhong amesema, wakati wa mkutano wa kilele wa FOCAC, China na Uganda zilithibitisha uamuzi wao wa kuinua uhusiano wao kuwa mkakati wa uhusiano wa ushirikiano wa kina wa pande zote ambao msingi wake ni maafikiano ya pamoja. Amesema katika miaka iliyopita, China imekuwa mwenzi muhimu wa Uganda, hususan katika kuendeleza sekta za miundombinu ya usafiri na nishati nchini humo.