Mara nyingi katika kipindi hiki tumekuwa tukizungumzia masuala mbalimbali kuhusu wanawake, kama alivyosema mwenzangu Pili, na tunafanya hivyo kwa sababu wanawake wanachukuliwa kama viumbe dhaifu, wasiojiweza, na wasioweza kufanya kazi ngumu ama kupewa majukumu makubwa. Lakini hali halisi ni kwamba, wanawake wana uwezo wa kufanya kazi sawa ama hata kuzidi wanaume, na pia wanawake wanajituma zaidi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku. Pia tumeshuhudia wanawake wakifanya kazi ambazo awali hazikuwa rahisi kufanywa na wanawake, na pia wametoa mchango mkubwa katika sehemu zao za kazi. Kwa upande wa sekta ya habari, wanawake wameendelea kufanya vema bila ya kukata tamaa, na wameonyesha uwezo wao mkubwa, licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Hivi karibuni, waandishi wa habari kutoka nchi za Afrika walikuja nchini China na kutembelea maeneo mbalimbali, ikiwemo Guangzhou, mkoa wa Guangdong. Miongoni mwao kulikuwa na wanahabari wanawake kutoka nchi za Kenya na Tanzania, ambao walikuwa na mengi ya kuzungumzia kuhusu mchango wa wanawake katika tasnia ya habari. Hivyo katika kipindi cha leo cha Ukumbi wa Wanawake, tumepata fursa ya kuzungumza na wanahabari wanawake ambao wameeleza mchango wa wanawake katika sekta ya habari na pia changamoto na mafanikio katika yao katika sekta hii.