Waziri Mkuu wa China asisitiza kufikia malengo ya maendeleo ya mwaka
2024-09-30 08:39:56| CRI

Waziri Mkuu wa China Li Qiang amesisitiza ulazima wa kufanya juhudi katika kutekeleza sera na mipango ya mamlaka kuu za nchi ili kufikia malengo ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa mwaka huu.

Waziri Mkuu Li ameyasema hayo alipokuwa akiongoza mkutano wa Baraza Kuu la Serikali, ulioweka mipango ya utekelezaji wa sera kadhaa za nyongeza zilizotolewa kwenye mkutano wa hivi karibuni wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China.

Mkutano huo ulitaka kuchukuliwa kwa hatua ili kutekeleza kikamilifu udhibiti wa jumla, kuhimiza ushirikiano kati ya sera mbalimbali, na kutatua changamoto kubwa katika shughuli za kiuchumi.

Mkutano huo uliweka mipango ya kuharakisha utekelezaji wa miradi muhimu 102 iliyotajwa kwenye mpango wa 14 wa maendeleo ya miaka mitano wa mwaka 2021 hadi 2025.