Wizara ya afya ya Rwanda imetangaza miongozo mipya ya kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya Marburg (MVD) baada ya idadi ya vifo kutokana na ugonjwa huo kuongezeka hadi kufika 8.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara hiyo Jumapili iliyopita, watu 26 wamethibitishwa kuambukizwa virusi hivyo na kati yao 18 wamewekwa karantini na kupewa matibabu. Wizara hiyo imewataka raia waepuke mawasiliano ya karibu na watu wenye dalili za ugonjwa huo, ikiwemo homa kali, maumivu makali ya kichwa na misuli, kutapika na kuhara.
Vituo vyote vya afya vimetakiwa kufuata kwa makini hatua za kinga na udhibiti wa maambukizi wakati wa kushughulikia wagonjwa wenye dalili za ugonjwa huo. Pia Wizara hiyo imetaka idadi ya watu wanaohudhuria mazishi ya waliofariki kwa ugonjwa huo isizidi 50.