MAADHIMISHO YA SHEREHE ZA MIAKA 60 YA CHUO KIKUU CHA LUGHA ZA KIGENI CHA TIANJIN, SANJARI NA MAADHIMISHO YA MIAKA 18 YA KOZI YA KISWAHILI
2024-10-01 11:47:07| cri

Tarehe 28 Septemba, Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Tianjin (TFSU) kilisherehekea miaka 60 tangu kuanzishwa kwake, na pia kuadhimisha miaka 18 ya kuanzishwa kwa Kozi ya Kiswahili. Wahitimu wamevuka milima na bahari wakitoka pembe mbalimbali duniani, wamerudi kwao kwa ajili ya kusherehekea pamoja, huku wakirejea na kukumbuka katika enzi za ujana wao.

Ili kusherehekea miaka 18 ya kuanzishwa kwa Kozi ya Kiswahili, Kitivo cha Utafiti wa Lugha za Asia na Afrika cha TFSU kimeandaa shughuli maalum ambayo ni mojawapo ya sherehe za miaka ya 60 ya chuo hicho. Wahitimu wengi wa Kozi ya Kiswahili wamehudhuria kwenye shughuli hiyo na “kurudi nyumbani”.

Katika ukuta wa kumbukumbu za sherehe za chuo hiki kutimiza miaka 60, mwangaza wa jua unamulika na kufanya maadhimisho haya kung'ara na kupendeza. Kampasi imepambwa kwa mapambo ya aina mbalimbali, huku maua yakishindana kwa uzuri, na sauti za furaha na shamrashamra zikieenea kila mahali. Wahitimu walishika maua mikononi mwao, wakitembea bega kwa bega ndani ya kampasi ya chuo. Nyuso zao zimejawa na furaha na shauku ya kurudi nyumbani.

Saa kumi na mbili na nusu jioni, sherehe ya kutimiza miaka 18 tangu kuanzishwa kwa Kozi ya Kiswahili ilianza rasmi. Viongozi wa Kitivo cha Utafiti wa Lugha za Asia na Afrika, walimu, wahitimu na wanafunzi wa Kozi ya Kiswahili walijumuika na kusherehekea pamoja.

Katika ukumbi wa chuo, muziki laini ulipopigwa, sherehe ikaaanza kwa mashamsham, ndirimo na sauti za shangwe.

Jukwaani, wanafunzi wapya wa Kozi ya Kiswahili waliimba kwa pamoja wimbo uitwao “Amani”, na melodi ya kupendeza ilisikika kana kwamba imepenya nyakati zote, ikileta hisia za uzuri wa amani na utulivu wa bara la Afrika. Kisha, dansi iliyochangamka iliwasha moto wa tukio, na wanafunzi walionyesha shauku zao kwa kutumia lugha zao za ishara. Kazi yao yenye ubunifu yaani shairi la kusifia TFSU ilisimulia maisha ya wanafunzi chuoni na hadithi zao. Wimbo maarufu wa Kiswahili “Jambo Bwana” na ngoma za Kiafrika zilizopigwa kwenye shughuli hiyo viliongeza shamrashamra na kukuza uzuri wa utamaduni wa Kiafrika kwa hali ya juu, hadi kufanya watazamaji wajisikie kama wako kwenye bara la Afrika.

Mbali na shughuli hiyo, wahitimu pia walialikwa kutoa risala wakieleza uzoefu wao na mawaidha ya masomo na ajira. Wahitimu walirudi darasani tena, wakizungukwa na wanafunzi wa chuoni. Walijibu kinaga ubaga maswali ya wanafunzi. Maneno yao yalifungua masikio ya wanafunzi na kuwatia ari ya kujifunza kwa bidii na kutoa mchango kwa ushirikiano kati ya China na Afrika.

Wahitimu bora wa Kozi ya Kiswahili walipewa medali katika sherehe. Medali sio tu kumbukumbu maalum, bali pia ni matarajio kutoka kwa viongozi, walimu na wanafunzi wa chuo. Mwishoni mwa tukio, wahitimu walijitokeza kuandika ujumbe wenye matumaini na shukrani zao kwenye ukuta wa maoni, na kila sentensi ilionyesha hisia zao.

Walimu wote wa Kozi ya Kiswahili walipoona “watoto” wao wakirudi nyumbani, walihisi furaha na fahari isiyokuwa na kifani. Katika miaka 18 iliyopita, kizazi baada ya kizazi cha wanafunzi wa Kiswahili katika chuo hiki kimehusika na kushuhudia maendeleo ya haraka ya Kozi ya Kiswahili na kupata mafanikio mengi ya kufurahisha. Katika mchakato wa kukua pamoja na chuo chao, wameweza kutimiza thamani na ndoto zao za maisha, na pia wamechangia katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla. Walimu wanatarajia kuwa, katika siku za mbele, Kozi ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Tianjin itaendelea kuandaa wahitimu wengi bora wa kimataifa, kuunga mkono maendeleo ya taifa, na kuimarisha daraja la urafiki kati ya China na Afrika.

Kozi ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Tianjin ilianzishwa rasmi mwaka 2006. Kisha mwaka 2007 ilianza kuandikisha wanafunzi wapya. Hadi sasa, Chuo hiki kimekuwa na wahitimu wa awamu saba wa shahada ya kwanza, na wahitimu wa awamu nne wa shahada ya uzamili, ambao wanashiriki kwa uchangamfu katika nyanja mbalimbali kama vile shughuli za Mambo ya Kigeni, Mawasiliano  ya Habari, Elimu, Biashara n.k. wakichangia katika maendeleo ya taifa na ushirikiano kati ya China na Afrika.
Heri ya Sikukuu ya Maadhimisho ya Miaka 18 ya Kozi ya Kiswahili na Heri ya Sikukuu ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Tianjin. Lugha ni amani, lugha ni umoja, lugha ni mshikamano kwa maendeleo ya taifa.