Kamati ya bunge la Kenya yakataa ombi la kutaka kupigwa marufuku kwa TikTok
2024-10-02 10:17:44| cri

Kamati ya bunge la Kenya imekataa ombi la kutaka kupigwa marufuku kabisa kwa TikTok nchini humo, badala yake imependekeza mamlaka za Serikali kukagua mara kwa mara utendaji wa mitandao ya kijamii.

Katika ripoti yake iliyowasilishwa Bungeni, Kamati ya Bunge la Taifa kuhusu Malalamiko ya Umma ilisema marufuku kamili ya TikTok itakandamiza uhuru wa vyombo vya habari na kujieleza.

"Marufuku ya moja kwa moja kwa TikTok nchini itakuwa na athari kubwa katika kuzuia uvumbuzi na ubunifu kati ya watumiaji ambao ni watunga maudhui.

"Marufuku itazuia haki ya uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari, haki zote za kikatiba katika demokrasia yetu," ripoti hiyo ilisema.

Kamati hiyo ilibainisha kuwa wakati nchi ikielekea kuimarisha uchumi wake wa kidijitali, kuzuia utendaji wa mitandao ya kijamii kutaondoa tija.