Toleo la 9 la Wiki ya Biashara ya China imeanza jana jumatano katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, ambapo maofisa waandamizi na makundi ya wawakilishi wa uwekezaji yakirejea wito wa kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya China na Kenya katika zama mpya.
Maonyesho hayo, sambamba na Maonyesho ya Kuijenga Afrika ya mwaka 2024 na Maonyesho ya Teknolojia ya Afrika ya mwaka 2024 yanayofanyika kuanzia Oktoba 2 hadi 4 mwaka huu, yamevutia washiriki 120, wakiwemo 85 kutoka China, ambao wanaonyesha bidhaa za ubora wa juu katika sekta mbalimbali za uchumi.
Waziri anayeshughulikia Vyama vya Ushirika na Biashara Ndogo na za Kati (MSMEs) wa Kenya Bw. Wycliffe Oparanya, amesema Wiki ya Biashara ya China imeibuka kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha biashara, uwekezaji na mawasiliano ya teknolojia kati ya Kenya na China.
Amesema Wiki hiyo itawapatia wafanyabiashara wadogo jukwaa la kuingia katika masoko mapya na mitaji, na pia njia zitakazoweza kuwasaidia kuchochea ukuaji wa biashara zao.