Mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Balozi Fu Cong ametoa wito wa kuboresha mfumo wa usimamizi wa dunia na kushughulikia ukosefu wa haki wa kihistoria uliofanywa kwa bara la Afrika.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu ushirikiano kati ya Umoja huo na Umoja wa Afrika (AU), Balozi Fu amesema nchi za Afrika zimeibuka kutoka utawala wa kikoloni na kutimiza uhuru wa kitaifa, na uanachama wao umeleta mageuzi katika Umoja wa Mataifa na kupanua kidhahiri ujumuishi wake.
Balozi Fu amesema, wakati wa Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la 79 la Umoja wa Mataifa uliofanyika wiki iliyopita, viongozi wa Afrika walitoa wito wa kuongeza kasi ya mageuzi ya mfumo wa uongozi wa kimataifa ili kuondoa ukosefu wa haki wa kihistoria ambao Afrika imeteseka nao kwa muda mrefu.