Ofisi ya Uratibu wa mambo ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema watu zaidi ya milioni 5 wa nchi 16 katika maeneo ya magharibi na kati mwa Afrika wameathiriwa na mafuriko mwaka huu, huku Chad, Niger na Nigeria zikiwa zimeathirika zaidi, zikiwa zinachangia zaidi ya asilimia 80 ya watu walioathiriwa.
OCHA imesema watu zaidi ya elfu moja wamekufa kutokana na mafuriko hayo na watu wasiopungua laki 7.4 wamekimbia makazi yao. Mbali na hayo, idadi kubwa ya nyumba, shule na vituo vya afya vimeharibiwa, na mashamba ya takriban ekari laki 5 yameathiriwa.
Ofisi hiyo imesema kutokuwepo kwa misaada ya kutosha, kutafanya mafuriko hayo kuleta changamoto za kijamii, haswa nchini Chad na Niger.