Rais Xi Jinping wa China na Kiongozi mkuu wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, Jumapili walipeana salamu za pongezi kwa kuadhimisha miaka 75 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Korea Kaskazini.
Katika salamu zake, Xi, alifahamisha kuwa miaka 75 iliyopita, China na Korea Kaskazini zilianzisha rasmi uhusiano wa kidiplomasia, na kufungua ukurasa mpya wa historia ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Xi aliongeza kuwa katika miaka 75 iliyopita, nchi hizo mbili zimesaidiana katika kuimarisha mamlaka ya watu na kulinda mamlaka ya kitaifa, kuimarisha mawasiliano na ushirikiano na kuendeleza ujenzi wa ujamaa. Pia wamefanya kazi kwa karibu ili kukuza amani na utulivu wa kikanda na kulinda usawa na haki ya kimataifa.
Kwa upande wake, Kim alisema miaka 75 iliyopita, pande hizo mbili zimeshikilia imani yao thabiti katika uhalali wa malengo yao, kushinda mitihani na changamoto mbalimbali, na kusonga mbele kwa ujasiri kwenye njia ya ujamaa. Kim pia alielezea imani yake kuwa watu wa China, chini ya uongozi wa CPC na Xi kama kiongozi wake mkuu, wataendelea kupata mafanikio mapya katika kujenga nchi ya kisasa ya ujamaa kwa pande zote.