Rwanda imeanza kufanya majaribio ya chanjo ya Marburg Jumapili, ikiwapa kipaumbele watumishi wa afya kama miongoni mwa juhudi za kuzuia kuenea kwa virusi vya Marburg nchini humo.
Waziri wa Afya wa Rwanda Sabin Nsanzimana alisema kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mjini Kigali Jumapili kuwa awamu ya kwanza ya chanjo ya majaribio inalenga watumishi wa afya, wafanyakazi wa hudumu ya dharura, na watu ambao wamewasiliana na wagonjwa waliothibitishwa kuwa na Marburg. Amesema hivi sasa wamepokea dozi 700 za chanjo inayotolewa na Taasisi ya Sabin Vaccine, ambayo tayari imeonekana kuwa na ufanisi katika nchi kama Uganda na Kenya, na chanjo nyingine zaidi zitawasili hivi karibuni ili kuendeleza juhudi za kulinda afya za watu.
Ili kuhakikisha uchunguzi kwa wakati, Rwanda imepanua uwezo wake wa kupima kwa kuanzisha maabara katika kila mkoa, ikiwa ni pamoja na Kigali. Katika hafla hiyo hiyo, mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Rwanda, Brian Chirombo, alisisitiza umuhimu wa kuwalinda watumishi wa afya, akibainisha kuwa virusi vya ugonjwa huo awali viliathiri wafanyakazi wa afya.