Misri Jumapili iliadhimisha miaka 51 tangu ilipopata ushindi kwenye Vita vya Oktoba ambavyo vinajulikana kama Vita kati ya Nchi za Kiarabu na Israel vya mwaka 1973, huku ikitaka kukomesha mapambano yanayosababisha vifo kwenye eneo hilo.
Rais Abdel-Fattah al-Sisi wa Misri alisema ushindi wa Misri kwenye vita hivyo utaendelea kuwa muda wa mabadiliko kwenye historia ya nchi hiyo, pia utakuwa alama ya ufahari na heshima yake.
Kwenye ukurasa wake wa Facebook, Sisi alisema katika siku hiyo, majeshi na viongozi wa Misri walionyesha moyo wao wa kujitolea mhanga kwa ajili ya kutwaa tena ardhi ya Sinai.
Wakati alipohudhuria kwenye mahafali ya vyuo vya kijeshi vya Misri siku ya Alhamisi Sisi alisema, maadhimisho ya mwaka huu ya ushindi wa Vita vya Oktoba yanafanyika katika kipindi kisichokuwa na utulivu kwenye historia ya eneo hilo, akitoa wito wa kujitoa upya kwenye haki na amani ya usawa.