Mafanikio na changamoto zinazowakabili wazee duniani
2024-10-07 10:45:50| CRI

Siku ya Kimataifa ya Wazee ni siku maalum kwa wazee kote duniani. Katika nchi nyingi, wanasiasa hutoa hotuba, haswa zile zinazohusiana na idara za serikali zinazoshughulikia wazee, katika kipindi hiki cha maadhimisho. Baadhi ya redio, televisheni au magazeti huweka mahojiano yanayohusu masuala mbalimbali ya wazee kama vile mafanikio waliyoyapata katika kujenga jamii bora.

Shirika la Afya Duniani (WHO), ambalo ni mamlaka ya Umoja wa Mataifa inayoongoza na kuratibu masuala yanayohusiana na afya, na makundi mengine yameshiriki kikamilifu katika kukuza ufahamu na umakini wa umma juu ya Siku ya Kimataifa ya Wazee. Majadiliano yanajikita katika mada kama vile: idadi ya watu wanaozeeka na utoaji wa huduma za afya za kutosha kwa wazee, kazi ya kujitolea, utunzaji wa kijamii, njia za kuwajumuisha zaidi wazee katika nguvu kazi na changamoto mbalimbali. Shirika la Afya Duniani (WHO) limetaja changamoto kubwa tatu zinazowakabili wazee ikiwemo huduma duni za afya, ukatili na uhakika wa kipato. Wakati wazee wakikabiliwa na changamoto hizo, asilimia 93 ya wenye zaidi ya umri wa miaka 60 hawamo katika mfumo wa hifadhi ya jamii. Hivyo katika kipindi cha ukumbi wa wanawake leo tutajadili mafanikio na changamoto zinazowakabili wazee duniani.