Mwaka mmoja baada ya kuongezeka kwa mzozo kati ya Israel na Palestina katika Ukanda wa Gaza, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alirejea tena wito wa kuwepo amani na haki katika Mashariki ya Kati.
Katika barua yake ya kila wiki iliyotolewa siku ya Jumatatu, rais Ramaphosa alisema hali ya mzozo inayozidi kuongezeka katika Mashariki ya Kati inatia wasiwasi mkubwa, na kuongeza kuwa jumuiya ya kimataifa haitamudu mzozo wa muda mrefu katika eneo hilo.
Ramaphosa alisisitiza msimamo wa Afrika Kusini kuhusu mzozo huo, akitoa wito wa kusitishwa mapigano mara moja, kitendo ambacho kitaleta ahueni kwa raia waliozingirwa, kumaliza mateso ya watu wa Gaza na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia wale wanaohitaji.
Kwa mujibu wa Ramaphosa, Afrika Kusini itawasilisha kumbukumbu ya ombi lake katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki The Hague baadaye mwezi huu ikiwa na ushahidi wa kina kuthibitisha kuwa Israel inatekeleza uhalifu wa mauaji ya halaiki huko Palestina.