Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Ukame nchini Kenya (NDMA) Jumatatu ilisema watu wasiopungua milioni moja wanakumbwa na ukosefu wa chakula nchini humo, na wanahitaji msaada wa kibinadamu.
Kwenye ripoti yake iliyotolewa Nairobi, NDMA ilisema watu wanaoathiriwa wako katika kaunti 23 kati ya kaunti 43, sehemu ambazo zinachukuliwa kama maeneo kame na nusu kame.
Mamlaka hiyo iligundua kuwa idadi ya watoto wenye umri wa miezi 6 hadi 59 wanaohitaji matibabu ya utapiamlo mkali imepungua kutoka 847,932 ya Februari hadi 760,488 mwezi Agosti. Wakati huohuo, idadi ya jumla ya wajawazito na wanawake wanaonyonyesha ambao wanahitaji matibabu kutokana na utapiamlo mkali imefikia 112,401.