Zaidi ya wajumbe 300 wakutana nchini Kenya kwa majadiliano ya biashara isiyo na mipaka
2024-10-08 09:16:46| CRI

Zaidi ya wajumbe 300 kutoka taasisi za mapato ya kodi barani Afrika, mashirika ya Umoja wa Mataifa, na jumuiya za kiuchumi za kanda ya Afrika wameanza kukutana Jumatatu mjini Nairobi, Kenya, ili kujadili njia za kukuza biashara isiyo na mipaka katika bara hilo.

Mkutano huo wa siku tatu wa Forodha na Biashara barani Afrika wenye kaulimbiu ya "Biashara Isiyo na Mipaka: Uwezeshaji Bora wa Biashara katika Enzi ya Dijitali" umewaleta pamoja washiriki kuangalia njia za kutumia teknolojia ili kuongeza uwezeshaji wa biashara barani Afrika.

Waziri Mkuu wa Kenya ambaye pia ni Waziri wa Masuala ya Kigeni na Diaspora Musalia Mudavadi alisema kuwa wasimamizi wa mipaka na forodha lazima watumie kikamilifu suluhu na mifumo inayoendeshwa na teknolojia inayorahisisha biashara na kuboresha uhamasishaji wa rasilimali za ndani.

Naye mkuu wa idara ya forodha, ushirikiano, uwezeshaji biashara, na usafiri katika Eneo la Biashara Huria la Afrika Gyang Demitta Chinwude, alisema kwa mazingira ya biashara yasiyo na mipaka, Afrika inahitaji miundombinu ya kidijitali ambayo inahitaji uwekezaji katika uunganishaji wa intaneti, majukwaa ya kidijitali, na mifumo salama ya mawasiliano ya kuvuka mipaka.