Afrika CDC yapongeza uzinduzi wa kampeni ya chanjo ya mpox nchini DRC
2024-10-08 09:15:54| CRI

Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kukinga Magonjwa (Afrika CDC) kimeipongeza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa kuzindua vyema kampeni yake ya chanjo ya mpox katika majimbo mawili yaliyopewa kipaumbele.

Katika taarifa ya Jumapili, CDC Afrika ilisema kuwa uzinduzi unaashiria hatua muhimu katika juhudi zinazoendelea za kudhibiti mlipuko wa mpox na kulinda idadi ya watu walio hatarini kote nchini.

Ikibainisha kuunga mkono juhudi za DRC kukabiliana na ugonjwa huo, hususan chanjo ya makundi yaliyo hatarini katika majimbo ya Equateur na Kivu Kaskazini nchini humo pamoja na washirika wengine wa kimataifa, CDC Afrika ilisema kampeni ya chanjo itafanyika na kwenye majimbo mengine hivi karibuni ili kuhakikisha upatikanaji wa kina zaidi.

Wiki iliyopita, CDC Afrika ilibainisha kuwa tangu kuanza kwa mwaka huu idadi ya jumla ya wagonjwa wa mpox barani Afrika imeongezeka hadi 34,297, wakiwemo 6,806 waliothibitishwa na vifo 866, huku DRC ikiwa kitovu cha mlipuko wa sasa wa ugonjwa huo barani Afrika.