Mjumbe maalumu wa China ahimiza kuziunga mkono nchi za Maziwa Makuu katika kuimarisha mshikamano na ushirikiano
2024-10-09 09:24:47| CRI

Mjumbe wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Fu Cong Jumanne alisema, jumuiya ya kimataifa inapaswa kuziunga mkono nchi za Maziwa Makuu katika kuimarisha mshikamano na ushirikiano, na kujenga mustakabali wa pamoja.

Fu Cong aliyasema hayo aliposhiriki kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la UM juu ya masuala ya eneo la Maziwa Makuu, akisema kuwa katika siku za hivi karibuni, nchi za Maziwa Makuu zinajitahidi kutafuta amani, usalama na maendeleo, na kuwa chachu kubwa katika kustawisha Mfumo wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na eneo la Maziwa Makuu.

Ameongeza kuwa wakati huohuo, eneo hilo bado linakabiliwa na changamoto mbalimbali, kama vile vurugu zinazoendelea na mgogoro mkubwa wa kibinadamu. Ametoa wito kwa nchi za kikanda kuimarisha mazungumzo na maafikiano, kushikilia kuishi pamoja kwa amani, kukabiliana na changamoto kwa pamoja, kudumisha usalama wa pamoja, kupunguza mgogoro wa kibinadamu, na kuhimiza maendeleo ya pamoja.