Chama cha Wafanyabiashara wa Chai Afrika Mashariki (EATTA) kilisema Jumanne kuwa Kenya imefuta bei ya chini kabisa ya chai yake inayouzwa katika soko kuu la mnada la kanda hiyo mjini Mombasa katika juhudi zake za kufanya bidhaa hiyo kuwa na ushindani wa kimataifa na kuongeza mauzo ya nje.
Mkurugenzi mkuu wa EATTA, chama cha wauzaji chai, madalali na wapakiaji, George Omuga, alisema katika taarifa iliyotolewa mjini Nairobi kwamba nchi hiyo inatupilia mbali bei ya chini kufuatia mashauriano kati ya wadau. Mwaka 2021 Kenya iliweka bei ya chini ya dola za Kimarekani 2.34 kwa kilo moja ya chai inayouzwa katika soko la nje ili kuepusha wakulima kupata hasara. Hata hivyo, hatua hiyo ilileta matokeo yasiyotarajiwa kwani wanunuzi walikwepa chai inayozalishwa katika nchi hiyo, na kusababisha mrundikano katika mnada huo.
Kufuatia kufutwa kwa bei hiyo ya chini, kampuni ya EATTA inayoendesha mnada ambapo chai kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki inauzwa, imewataka wadau wa mnyororo wa thamani kuhakikisha uwazi.