Rais wa Uganda asema angependa kusuluhisha mzozo wa Sudan
2024-10-09 09:13:58| CRI

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema angependa kuwa mpatanishi wa amani katika mzozo unaoendelea nchini Sudan ambao umesababisha vifo vya maelfu ya watu na mamilioni ya wengine kuyahama makaazi yao.

Rais Museveni amesema hayo wakati alipokutana na Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia suala la Sudan Ramtane Lamamra. Rais Museveni ameongeza kuwa yuko tayari kusuluhisha mzozo kama watakubali, na kuzitaka pande zinazozozana kukubaliana kusitisha mapigano na kukabidhi madaraka kwa watu wa Sudan.

Lamamra alimhakikishia Museveni kwamba Umoja wa Mataifa utamuunga mkono kutatua mzozo huo.

Wakati huohuo Mtandao wa Madaktari wa Sudan usio wa kiserikali jana ulitangaza kuwa takriban watu 20 wameuawa na wengine watatu kujeruhiwa katika shambulizi lililofanywa na Wanajeshi wa Msaada wa Haraka (RSF) katika kijiji kimoja cha Jimbo la Kordofan Kaskazini magharibi mwa Sudan. Mtandao huo haukutoa maelezo ya ziada, na RSF bado haijatoa maoni yoyote kuhusu shambulizi hilo.