Utafiti waonesha Afrika yapoteza dola bilioni 4.2 kila mwaka kutokana na vyombo vya habari vya Magharibi kuitangaza vibaya Afrika
2024-10-11 08:47:56| CRI

Kwa mujibu wa utafiti uliotangazwa Alhamisi, habari za kuichafua Afrika, hasa zinazotangazwa na vyombo vya habari vya Magharibi, zinalifanya bara hilo lipoteze wastani wa dola za kimarekani bilioni 4.2 kila mwaka.

Utafiti huo uliofanywa na Africa Practice, kampuni ya ushauri ya kimkakati, na Africa No Filter, kampuni ya ushawishi wa utetezi, unalaumu vyombo vya habari vya Magharibi kwa kutoa taswira potofu ya bara hilo na kuzorotesha imani ya wawekezaji na kudumaza ukuaji.

Utafiti huo uliopewa jina la "Gharama ya Fikra Potofu ya Vyombo vya Habari kwa Afrika," unaangazia michakato ya uchaguzi nchini Kenya, Nigeria, Afrika Kusini na Misri na habari potofu kutoka vyombo vikubwa vya habari kutoka Global North. Umesema hasara ya dola bilioni 4.2 inayosababishwa na habari za kupotosha za vyombo vya habari kila mwaka inaweza kufadhili elimu ya watoto milioni 12 wa Afrika, na kutoa chanjo kwa zaidi ya watoto milioni 73, idadi ambayo ni kubwa kuliko ukichanganya wakazi wote wa Angola na Msumbiji.

Afisa mkuu mtendaji wa Africa Practice, Marcus Courage, alisema utafiti umesisitiza udharura wa kupinga dhana potofu kuhusu Afrika inayoendelezwa na vyombo vya Magharibi, vilivyojikita katika ubaguzi wa rangi na mitazamo ya kikabila.