Maisha ya wazee katika zama za kidijitali
2024-10-12 09:00:03| CRI

    Suala la usalama katika mitandao ya kijamii limekuwa likizungumzwa mara kwa mara, lakini bado kuna changamoto kadhaa zinazotokana na matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watu wa jinsia zote na umri wote. Katika vipindi vyetu vilivyopita tumekuwa tukijadili suala hili na kuzungumza na washusika kuhusiana na changamoto zinazotokana na matumizi ya mitandao ya kijamii, ikiwemo kunyanyaswa kijinsia, kudhalilishwa, na hata taarifa za mhusika kutumika isivyo. Katika hali kama hiyo, wazee wanajikuta kwenye changamoto kubwa kwa kuwa mengi yanayojitokeza kwenye mitandao ya kijamii ni ya kitaalamu zaidi na wengi wao hawana ujuzi mkubwa katika kutumia mitandao hiyo, na hivyo kujikuta wakidanganywa kununua vitu ambavyo havina ubora, na hata kutoa kiasi kikubwa cha pesa kwa matapeli wanaotumia mitandao hiyo.

    Na kama tunavyojua Oktoba Mosi kila mwaka ni Siku ya Wazee Duniani, na tarehe 9 mwezi wa 9 kwa kalenda ya kilimo ya China, ambayo kwa kalenda ya kawaida ni Oktoba 11 ambayo ni jana kwa mwaka huu, ni Siku ya Wazee nchini China, siku hiyo kwa Kichina inaitwa siku ya Chongyang. Wachina wa zama za kale waliamini kuwa, namba 9 ni ishara ya baraka, na tarehe 9 mwezi wa 9 ni siku inayoweza kuleta baraka mara dufu. Katika zama za sasa, wachina wameona siku hiyo ya tarehe 9 mwezi wa 9, namba ambayo kwa kichina inaitwa Jiu, inatamkwa sawa na neno la kichina “daima milele” yaani Jiujiu, hivyo wachina waliamua siku hiyo kuwa ni siku ya wazee, maana ya sikukuu hiyo imeonesha wachina wanaoheshimu, kuwapenda na kuwatakia wazee waishi maisha marefu. Sasa katika kuadhimisha siku hii, kipindi hiki cha Ukumbi wa Wanawake leo hii, tunaangalia changamoto wanazokumbana nazo wazee katika matumizi ya mitandao ya kijamii.