Bodi ya Utalii nchini Kenya (KTB) imezindua kampeni itakayotumia taasisi zake za nje ya nchi kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchi hiyo.
Ofisa Mkuu Mtendaji wa Bodi hiyo, June Chepkemei amesema, Wakenya wanaoishi nje ya nchi watachukua nafasi kubwa katika utekelezaji wa kampeni hiyo inayoitwa “Diaspora mmoja, Mtalii Mmoja,” ambayo inalenga kuwatumia raia zaidi ya milioni 3 wa Kenya wanaoishi nje ya nchi kusaidia kutangaza soko la utalii nchini humo ndani ya nchi wanazoishi.
Ofisa huyo amesema kampeni hiyo inatarajiwa kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchi hiyo, na kuthibitisha nafasi ya Kenya kama kituo bora cha utalii. Pia amesema, kampeni hiyo itawawezesha Wakenya wanaoishi nje ya nchi kutangaza utalii kupitia mitandao yao ya kijamii, na watafanya hivyo kwa kushirikiana na Bodi hiyo.