Msomi wa Somalia: Uhusiano kati ya Somalia na China kuweka mfano wa kuigwa wa ushirikiano kuelekea ustawi wa pamoja
2024-10-14 15:46:25| CRI

Kwenye Mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika mwezi Septemba 2024 mjini Beijing, Rais Xi Jinping wa China na mwenzake wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud waliamua kuinua uhusiano wa nchi zao hadi kufikia ngazi ya Uhusiano wa Wenzi wa Kimkakati. Mshauri mwandamizi wa Waziri Mkuu wa Somalia Dkt. Hodan Osman Abdi, amesema uamuzi huu unaashiria kuwa urafiki wa muda mrefu na uhusiano wa karibu kati ya Somalia na China uliokita mizizi katika msingi wa historia inayofanana, kuheshimiana na ruwaza ya pamoja kwa siku zijazo, sasa umeingia kwenye hatua mpya ya kimkakati.

Dkt. Hodan Abdi amesema, kuinuka kwa uhusiano kati ya Somalia na China ni hatua muhimu inayotokana na mawasiliano ya karibu yaliyokuwepo kwa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili, ambazo sasa zinajitahidi kujenga ushirikiano wa kimkakati unaotafuta ukuaji wa pamoja na ustawi wa pamoja. Kwa upande wa Somalia, hatua hiyo italeta manufaa makubwa. Akimnukuu Rais Hassan Sheikh Mohamud, Dkt. Hodan amesema Somalia iliyoko katika kipindi cha mageuzi na mabadiliko, inahitaji ujuzi, teknolojia na uzoefu wa China katika kujenga upya miundombinu na kuboresha raslimali watu, na kwamba Somalia inaichukulia China kuwa ni mshirika wa kuaminika, na mustakbali wa Somalia unategemea ushirikiano wake na wenzi wa kuaminika ikiwemo China, wakati nchi hiyo inapojitahidi kudumisha utulivu na kukuza uchumi.

Dkt. Hodan amesema, katika miongo kadhaa ijayo, uhusiano kati ya Somalia na China huenda utakuwa mfano wa kuigwa wa kujenga ustawi wa pamoja. Urafiki wa muda mrefu kati ya pande hizo mbili uliojengwa kwenye msingi wa kushikamana na kuheshimiana, sasa unatarajia kukumbatia fursa mpya katika siku zijazo.