Watu 23 wameuawa na wengine zaidi ya 40 kujeruhiwa katika shambulio la anga lililolenga soko kuu lililoko kusini mwa mji mkuu wa Sudan, Khartoum, jumamosi iliyopita.
Taarifa iliyotolewa na kundi la watu wanaojitolea linaloitwa Chumba cha Dharura cha Khartoum Kusini imesema, tukio hilo lilitokea wakati ndege ya kivita iliposhambulia kwa mabomu soko kuu la Al-Souk Al-Markazy lililoko Khartoum jumamosi mchana.
Mpaka sasa, hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na shambulio hilo.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA), mapigano makali yalizuka kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha Mwitikio wa Haraka (RSF) mwezi April mwaka jana, na kusababisha vifo vya watu karibu 20,000 na kujeruhi maelfu wengine, na mamilioni wengine kuwa wakimbizi.